Vita ya ushuru baina ya kanada na marekani
September 10, 2026 Posted by Yasin Mohamed
Washington imeongeza makali katika vita ya kibiashara na Kanada. Katika hatua mpya iliyotangazwa sasa, Marekani imeamua kuzuia uagizaji wa baadhi ya bidhaa kutoka Kanada, hatua inayotarajiwa kuanza kutekelezwa Septemba 29, 2026.
Miongoni mwa bidhaa zitakazoathirika ni vileo mbalimbali, baadhi ya bidhaa za maziwa, pamoja na pikipiki zenye injini kubwa. Hatua hii imekuja baada ya Kanada kuweka ushuru wa kulipiza kisasi kwa bidhaa za Marekani zenye thamani ya takriban dola bilioni 27.6 za Kanada, kuanzia Septemba 8.
tunaelekea wapi?
Sep 10, 2026 posted by Yasin Mohamed
Kanada na Marekani wamekuwa majirani na washirika wa karibu wa kibiashara kwa muda mrefu sana. Uhusiano huo uliimarishwa zaidi mwaka 1989, wakati Mkataba wa Biashara Huria kati ya nchi hizo mbili ulipoanza kutumika, na baadaye mwaka 1994 kupitia NAFTA, ambayo iliunganisha zaidi masoko ya Kanada, Marekani na Mexico.
Kwa miongo kadhaa, bidhaa, malighafi, magari, chakula, nishati na huduma zimekuwa zikivuka mpaka kati ya nchi hizi mbili kwa kiwango kikubwa. Mfumo huo ulionekana kuwa sehemu ya kawaida ya maisha ya kiuchumi ya Amerika Kaskazini.
Kwa hiyo, kwa muda mrefu, hakukuwa na sababu kwa mwananchi wa kawaida kufikiria sana kuhusu mpaka huo wa kibiashara. Bidhaa zilienda huku na kule, viwanda vikafanya kazi kwa kutegemeana, na biashara ikaendelea kama sehemu ya maisha ya kila siku. Maisha yalikuwa shwaari.
Lakini hali hiyo ya utulivu sasa imevurugika.
Leo tunashuhudia kile kinachoonekana kama vita ya ushuru—Marekani ikiweka ushuru kwa baadhi ya bidhaa za Kanada, Kanada nayo ikijibu kwa kuweka ushuru kwa bidhaa za Marekani. Mnamo Septemba 8, 2026 hapo juzi tu, Kanada ilianza kutekeleza ushuru wa kulipiza kisasi kwa bidhaa za Marekani zenye thamani ya takriban dola bilioni 20 za Kanada, huku Marekani ikitangaza hatua zaidi dhidi ya bidhaa za Kanada.
Lakini hapa ndipo jambo linapokuwa la kusikitisha kwa Kanada.
Kanada ni nchi yenye uchumi mdogo kuliko Marekani, na imejenga sehemu kubwa ya biashara yake kuelekea soko la Marekani. Mwaka 2025, karibu asilimia 72 ya bidhaa zote za Kanada zilizouzwa nje zilienda Marekani.
Hiyo ina maana kwamba Kanada inapopigana kibiashara na Marekani, haiwezi kujitenga na madhara hayo kwa urahisi. Kampuni za Kanada zinapopoteza soko au kukumbana na gharama kubwa za ushuru, madhara yanaweza kuonekana katika ajira, uwekezaji na hatimaye bei ambazo mwananchi analipa dukani.
Na hapa ndipo mwananchi wa kawaida anapoingia katika picha hii.
Ushuru unaweza kuonekana kama jambo linalohusu serikali na wafanyabiashara wakubwa, lakini gharama yake inaweza kufika kwa mlaji. Ikiwa bidhaa, malighafi au sehemu za bidhaa zinatoka Marekani na sasa zina gharama kubwa zaidi, mfanyabiashara anaweza kulazimika kuongeza bei. Ndiyo maana vita hii inaweza kugusa vitu tunavyonunua kila siku—kuanzia chakula na mavazi hadi vifaa vya nyumbani na bidhaa nyingine.
Marekani nayo haiwezi kusema kwamba haina cha kupoteza. Biashara kati ya nchi hizi mbili ilikuwa na thamani ya takriban dola bilioni 872 mwaka 2025. Hivyo uchumi wa nchi hizo mbili umefungamana sana. Na viongozi husika kwa upande zote mbili wanjua hayo.
Lakini tofauti ni kwamba Marekani ina soko kubwa la ndani, watu wengi zaidi na uchumi mkubwa zaidi. Kwa hiyo, kwa muda mrefu, Marekani inaweza kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kustahimili mshtuko wa kupungua kwa biashara na Kanada kuliko Kanada inavyoweza kustahimili kupoteza sehemu kubwa ya soko lake la Marekani.
Hilo ndilo linalofanya hali hii kuwa hatari zaidi kwa Kanada.
Je, nani ana makosa? Hilo ni swali la kisiasa ambalo pande zote mbili zinaweza kulijibu kwa mtazamo wao. Lakini jambo moja ni wazi: vita ya ushuru haina mshindi wa haraka. Kanada inaweza kulipiza kisasi, Marekani inaweza kuongeza shinikizo, lakini mwisho wa siku biashara inapungua, gharama zinaongezeka na wananchi wanaweza kuanza kuuliza: “Kwa nini sisi ndio tunalipa gharama ya vita ambayo hatukuianzisha?”
Labda somo kubwa kwa Kanada ni kwamba uhusiano huu wa muda mrefu umetufanya kutegemea sana soko moja. Serikali sasa inazungumzia kuongeza biashara na Ulaya na masoko mengine ili kupunguza utegemezi huo. Ripoti ya serikali ya Kanada inaonyesha kwamba mwaka 2025 mauzo ya Kanada kwenda masoko yasiyo ya Marekani yaliongezeka kwa asilimia 11.1.
Hilo linaweza kuwa suluhisho la muda mrefu. Lakini kwa muda mfupi, suluhisho bora zaidi bado ni mazungumzo na makubaliano, kwa sababu Kanada na Marekani si maadui—ni majirani, washirika na uchumi ambao umeunganishwa kwa karibu sana.
Vita ya ushuru inaweza kuanza Washington na Ottawa, lakini gharama yake inaweza kuishia kwenye pochi ya mwananchi wa kawaida.